Breaking


Jumatatu, 5 Oktoba 2026

MAREKANI: WAKILI AIOMBA HUKUMU YA KIFO YA CHRISTA PIKE IBADILISHWE KUWA KIFUNGO CHA MAISHA


MAREKANI


Wakili wa Christa Pike, Stephen Ferrell, ameiomba Serikali ya Tennessee kubadilisha hukumu ya kifo ya mteja wake na kuwa kifungo cha maisha, kufuatia kushindikana kwa utekelezaji wa hukumu hiyo.

Ferrell ameiambia CNN kuwa Pike bado yuko hospitalini na anasaidiwa kupumua kwa mashine (ventilator), huku hali yake ya kiafya ikiendelea kuwa mbaya. Kwa mujibu wa wakili huyo, madaktari bado hawajaweza kubaini hatma ya afya yake, na huenda ikachukua siku kadhaa kujua iwapo atapata nafuu.

Pike, mwenye umri wa miaka 50, alihukumiwa kifo kwa kuhusika na mauaji ya Colleen Slemmer, aliyekuwa na umri wa miaka 19, mwaka 1995. Wakati wa tukio hilo, Pike alikuwa na umri wa miaka 18.

Pike alihukumiwa pamoja na mpenzi wake wa wakati huo, Tadaryl Shipp, ambaye yeye alihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Utekelezaji wa hukumu ya Pike ulifanyika Tennessee, lakini haukukamilika kama ilivyotarajiwa baada ya maafisa kumpa dawa ya pentobarbital kwa ajili ya kutekeleza hukumu hiyo. Licha ya kupewa dozi mbili, Pike hakufariki na baadaye alipelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Taarifa zinaeleza kuwa tangu apelekwe hospitalini, Pike hajapata fahamu na anaendelea kusaidiwa kupumua kwa mashine.

Baada ya tukio hilo, Gavana wa Tennessee, Bill Lee, aliamuru uchunguzi ufanyike ili kubaini kilichosababisha utekelezaji huo kushindikana. Pia, utekelezaji mwingine wa hukumu za kifo uliokuwa umepangwa kufanyika mwaka huu ulisitishwa.

Akizungumza kuhusu hali ya mteja wake, Ferrell amesema Pike tayari ametumikia takribani miaka 30 gerezani na amepitia hali ngumu wakati wa jaribio la kutekeleza hukumu yake.

Kwa sababu hiyo, wakili huyo amemuomba Gavana Bill Lee kuzingatia kubadilisha hukumu ya kifo ya Pike kuwa kifungo cha maisha.

Una maoni gani kuhusu ombi la wakili huyo? Je, unadhani hukumu ya kifo inapaswa kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha katika mazingira kama haya? Tujulishe maoni yako kwenye sehemu ya maoni.

Chanzo: CNN


Hakuna maoni: