Breaking


Jumatatu, 5 Oktoba 2026

ZUNGU AFUNGUA JUKWAA LA WANAWAKE LA IPU, ATOA WITO WA KUONGEZA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA UONGOZI


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amefungua Mkutano wa Jukwaa la Wanawake wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) leo Oktoba 5, 2026 katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Akizungumza wakati akifungua Mkutano huo, Zungu alisema maendeleo yaliyopatikana katika kuongeza uwakilishi wa wanawake mabungeni yanatia moyo. 

“Kwa mfano, nchini Tanzania, uwakilishi wa wanawake bungeni ni asilimia 39.5,” amesema. 

Hata hivyo, alisema uwakilishi pekee hautoshi hivyo Mabunge Wanachama wa IPU yanapaswa kuendelea kushughulikia vikwazo vinavyoathiri ushiriki madhubuti, uongozi na ushawishi wa wanawake katika michakato ya kisiasa na kibunge.

“Tunapokutana hapa Tanzania, hebu tuthibitishe tena kuwa mabunge yanayoshirikisha makundi yote ni mabunge imara zaidi,” amesema.

Amesema kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika nyanja ya kisiasa kunaimarisha taasisi za kidemokrasia na kuchangia katika utawala unaowakilisha vyema wananchi na kujali mahitaji yao.

Amewahimiza washiriki kutumia Jukwaa hilo kubadilishana uzoefu kwa uwazi, kujenga ushirikiano na kubainisha hatua madhubuti za kuchukua katika mabunge ya nchi Wanachama.

Aliongeza kuwa kuondoa vikwazo vya kimfumo na kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa ya kushiriki katika maamuzi, kunajenga imani katika taasisi na kufungua fursa za pamoja zinazohitajika ili kujenga dunia yenye haki na inayoshirikisha watu wote. 

Ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 153 wa IPU unatarajiwa kufanyika baadaye hii leo jioni.

Hakuna maoni: