Breaking


Jumatatu, 19 Oktoba 2026

MCHUNGAJI PAUL MACKENZIE KUSOMEWA HUKUMU KATIKA MAUAJI YA SHAKAHOLA



Mchungaji mwenye utata kutoka nchini Kenya, anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ya watoto 191, katika mojawapo ya matukio mabaya zaidi yanayohusishwa na madhehebu ya kidini katika historia, anatarajiwa kusomewa hukumu yake leo.

Mchungaji Paul Mackenzie, anadaiwa kuwaongoza mamia ya wafuasi wake katika msitu mmoja Pwani ya Kenya, na kuwashawishi kufunga hadi kufa ili wakutane na Yesu.

Aidha, mchungaji huyo pia aliwashawishi wafuasi wake kukataa matibabu ya kisasa na hata elimu.

Katika mahubiri yake, mara nyingi alionya kuwa mwisho wa dunia ulikuwa umekaribia na kwamba shetani alikuwa ameingia katika maisha ya kisasa.

Mwaka wa 2023, polisi waligundua miili iliyokuwa imeoza ya wafuasi wake zaidi ya 400 katika msitu wa Shakahola, Pwani ya Kenya, hali iliyochochea uchunguzi kufanywa na kufunguliwa kwa kesi mahakamani.

Mackenzie amekanusha mashtaka yote dhidi yake, akidai kuwa hakuwalazimisha wafuasi wake kufunga hadi kufa, lakini Polisi bado wanafanya vipimo vya vinasaba vya DNA ili kutambua mabaki ya waliofariki kabla ya familia zao kuruhusiwa kuyazika. 

Hakuna maoni: