Breaking


Jumatatu, 19 Oktoba 2026

TPSF YAMTEUA DEOGRATIUS MASSAWE KUWA MKURUGENZI MKUU



Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania, TPSF, limemtangaza Bw. Deogratius Massawe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirikisho hilo, kufuatia kukamilika kwa Mkutano Mkuu wa 24 wa mwaka, uliofanyika Oktoba 16, 2026.


Massawe ameteuliwa kushika nafasi hiyo baada ya kuhudumu kama Kaimu Mkurugenzi Mkuu tangu Oktoba mwaka 2025, kipindi ambacho amekuwa akiongoza utekelezaji wa mageuzi ya taasisi hiyo, kuimarisha mwelekeo wa kimkakati na kuweka mazingira bora zaidi ya TPSF kutekeleza majukumu yake ya kuwakilisha maslahi ya sekta binafsi nchini.


Uteuzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za shirikisho hilo za kuimarisha utetezi wa maslahi ya wafanyabiashara, kukuza mazungumzo kati ya serikali na sekta binafsi, pamoja na kuendeleza mazingira rafiki na yenye ushindani kwa shughuli za biashara nchini Tanzania.


Kupitia taarifa iliyotolewa kwa niaba ya Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania, Rais wa TPSF, Bi. Angelina Ngalula, amempongeza Massawe kwa uteuzi huo na kumtakia mafanikio katika kipindi chake cha uongozi.


Ngalula amesema uteuzi huo unafungua ukurasa mpya kwa shirikisho hilo katika kuendeleza ukuaji, mageuzi ya taasisi na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.


TPSF ni taasisi inayowakilisha maslahi ya sekta binafsi nchini, ikifanya kazi ya kukuza ushirikiano kati ya wafanyabiashara na serikali katika masuala yanayohusu maendeleo ya biashara na uchumi.


Uteuzi wa Deogratius Massawe unakuja wakati ambapo sekta binafsi inaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kukuza uwekezaji, kuongeza shughuli za kiuchumi na kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini Tanzania.

Hakuna maoni: