MEYA wa Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, Dkt. Nicas Mawazo, amewataka wawekezaji kushirikiana na Serikali kuchangia maendeleo ya jamii, hususan kuboresha miundombinu ya elimu na mazingira.
Akitembelea viwanda vya Qounquer Investment Company Ltd kinachozalisha tishu na Ufresh Food Ltd kinachozalisha juisi, vilivyopo Kongowe, ameeleza ushirikiano huo utasaidia kutatua changamoto zinazokabili shule, ikiwemo Sekondari ya Mwambisi.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake, hivyo wawekezaji wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia maendeleo ya jamii zinazowazunguka.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko na Mahusiano wa Qounquer Investment Company Ltd, Robert Baclay, amesema kiwanda hicho kinachangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni la Sekondari ya Mwambisi, huku Ufresh Food Ltd ikichangia mabati 500.
Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, Byson Mpogoza, amefafanua viwanda vinapaswa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Sura ya 191, pamoja na kanuni zake zinazohusu udhibiti wa uchafuzi na usimamizi wa maji taka.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni