Breaking


Jumamosi, 10 Oktoba 2026

VIONGOZI WAWASILI JIJINI BANGKOK KUSHIRIKI MIKUTANO YA MWAKA YA IMF NA BENKI YA DUNIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, ambaye pia ni Gavana Mbadala (Alternate Governor) anayewakilisha Tanzania katika Benki ya Dunia, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambaye pia ni Gavana Mbadala anayewakilisha Tanzania katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Emmanuel Tutuba, wamewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Suvarnabhumi, jijini Bangkok, nchini Thailand.

Viongozi hao wamewasili wakiambatana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, kwa ajili ya kushiriki Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika nchini Thailand kuanzia tarehe 12 hadi 18 Oktoba 2026.

Tanzania ni mwanachama wa taasisi hizo muhimu za kifedha duniani, ambazo ni wadau wakuu katika kusaidia juhudi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kupitia ushirikiano wa kifedha, kiufundi na kisera. 

Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano hiyo ya Mwaka, unaongozwa na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ambaye ni Gavana  anayeiwakilisha Tanzania katika Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.

Hakuna maoni: