Breaking


Alhamisi, 5 Novemba 2026

PAC YATAKA UCHUNGUZI UFANYIKE KUHUSU DOSARI MIRADI YA VIWANJA VYA MICHEZO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu dosari zilizobainika katika miradi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Arusha, Uhuru na Benjamin Mkapa, huku ikisisitiza kurejeshwa kwa fedha zilizolipwa bila stahili na kuwawajibisha wote waliohusika.

Hatua hiyo imekuja baada ya Kamati kupitia taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zilizobainisha changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwemo ongezeko kubwa la gharama, kasoro katika taratibu za zabuni, udhibiti hafifu wa ubora wa kazi pamoja na malipo ya kazi ambazo hazikukamilishwa au kutekelezwa.

GHARAMA ZA UWANJA WA ARUSHA ZAPANDA KWA ASILIMIA 81

Katika mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Arusha, Kamati imebaini kuwa makadirio ya gharama za mradi huo yaliongezeka kutoka Shilingi bilioni 187 hadi Shilingi bilioni 338.54.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 81 ya gharama za awali, jambo lililozua maswali kuhusu usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha katika utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, ilibainika kuwa usanifu wa awali wa uwanja huo haukuzingatia kikamilifu mahitaji ya viwango vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa Daraja la Nne.

KASORO ZAIBULIWA KATIKA GHARAMA ZA UWANJA WA UHURU

Kwa upande wa Uwanja wa Uhuru, Kamati imebaini ongezeko kubwa la gharama za ununuzi wa vifaa vya mfumo wa mwanga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gharama za vifaa hivyo zilipanda kutoka Shilingi milioni 185.8 hadi Shilingi bilioni 1.85.

Pia, Kamati imeeleza kuwa mzabuni aliyetoa bei ya juu kwa Shilingi milioni 865 ndiye aliyechaguliwa kutekeleza kazi hiyo, huku CAG akibaini kutokuwepo kwa nyaraka za kutosha kuthibitisha kuwa mzabuni aliyetoa bei ya chini hakuwa na uwezo wa kutekeleza zabuni hiyo.

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu uwazi, ushindani na uzingatiaji wa taratibu katika mchakato wa kumpata mzabuni wa mradi huo.

PAC YATAKA HATUA ZA UWAWAJIBIKAJI

Kutokana na dosari hizo, Kamati ya PAC imesisitiza umuhimu wa Serikali kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha fedha za umma zinalindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Miongoni mwa hatua zinazotakiwa ni kufanya uchunguzi wa kina, kurejesha fedha zilizolipwa bila stahili na kuwawajibisha watu au taasisi zitakazobainika kuhusika na ukiukwaji wa taratibu.

Kamati pia imeonesha umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa miradi ya umma, udhibiti wa gharama na uhakiki wa ubora wa kazi ili kuzuia changamoto zinazoweza kusababisha upotevu wa fedha za Serikali.

Miradi ya viwanja vya michezo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya miundombinu ya michezo nchini. Hivyo, usimamizi madhubuti wa fedha na utekelezaji wake ni muhimu ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha zinazotumika.


Hakuna maoni: