Breaking


Alhamisi, 5 Novemba 2026

WIZARA YA AFYA YAWEKA MSUKUMO WA UTAYARI KUJIANDAA KUKABILIANA NA EBOLA MBINGA



Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Shirika la Afya Duniani (WHO), leo Novemba 4, 2026, imefanya tathmini ya utayari wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga (Mbuyula) na Kituo cha Afya binafsi cha St. Vincent katika kukabiliana na Ebola, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya katika kutambua, kujikinga na kudhibiti maambukizi.

Akizungumza wakati wa tathmini hiyo, Mratibu wa Huduma za Tiba Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Yona Mwakabumbe, amesema wamefurahishwa na ujio wa timu ya Wizara ya Afya iliyofika katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.

Amesema vituo hivyo vimechaguliwa kwa kuwa vinahudumia wananchi wengi, hivyo ni muhimu kuwa na utayari wa kutambua mapema mtu anayehisiwa kuwa na maambukizi na kumtenga kabla hajachanganyika na watu wengine.

Ameongeza kuwa tathmini hiyo imewezesha kubaini maeneo yaliyofanya vizuri na yale yanayohitaji maboresho, huku timu ya Mbinga ikitoa ushirikiano mzuri kufanikisha zoezi hilo.

Kwa upande wake, Dkt. Morgan Bitwi, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, amesema wameupokea vizuri ujio wa wataalamu hao ambao umewawezesha kupata maelekezo sahihi kuhusu namna ya kujikinga, kumkinga mtu anayehisiwa kuwa na maambukizi na taratibu za kumpokea mgonjwa.

Aidha, amesema wataalamu hao wamewasaidia kubaini maboresho yanayohitajika katika maandalizi ya maeneo maalumu ya kuwatenga wagonjwa wa magonjwa ya milipuko ili kuhakikisha wanahudumiwa katika mazingira salama.

Dkt. Bitwi ameshukuru kwa elimu na maelekezo waliyoyapata, akiahidi kuwa halmashauri itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kwa wakati ili kuimarisha utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya katika kukabiliana na Ebola na magonjwa mengine ya milipuko.

Hakuna maoni: