Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Bw. Gilead Teri, amesema kuwa kukamilika kwa Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kutaongeza thamani ya biashara ya mauzo kwa zaidi ya shilingi bilioni 300 kila mwaka.
Akizungumza kuelekea uzinduzi rasmi wa kituo hicho unaotarajiwa kufanyika tarehe 2 Agosti mwaka huu, Bw. Teri alieleza kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kituo hiki ni hatua muhimu kwa maendeleo ya biashara na uchumi wa nchi. Tunatarajia kuona ongezeko kubwa la mauzo, fursa za ajira, pamoja na mapato ya Serikali kupitia kodi,” alisema Teri.
Aidha, alizihimiza halmashauri nyingine nchini kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kutekeleza miradi kama hiyo, akisisitiza kuwa hatua hiyo italeta uchechemuzi wa kiuchumi na kuimarisha pato la taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EACLC, Bi. Cathy Wang, aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na kituo hicho ili kujikwamua kiuchumi.
“Tunapoweka miundombinu ya kisasa kama hii, ni wajibu wa wafanyabiashara kuitumia kwa tija. Hii ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kushiriki kikamilifu katika biashara za kikanda na kimataifa,” alisisitiza Wang.
Kituo hicho kilianza kutekelezwa mwezi Mei 2023 na kimekamilika mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 282.7. Kinatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira rasmi 15,000 pamoja na ajira zisizo rasmi 5,000.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni