Kupitia ujumbe wake, Ahmed Ally amesema matokeo hayo yanapaswa kuchukuliwa kama sehemu ya mchezo wa soka, huku akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kulaumiana au kutafuta mchawi baada ya timu hiyo kupoteza.
“Macho mbele Wana Simba wenzangu. Hii imeshapotea, haikuwa riziki na hatuna sababu ya kulaumiana wala kutafuta mchawi,” amesema Ahmed Ally.
Ameongeza kuwa katika baadhi ya vipindi vya mchezo Simba ilikuwa na ubora lakini haikuweza kuutumia kupata matokeo, huku Yanga ikitumia nafasi zake vizuri na kuibuka na ushindi.
“Kuna nyakati tulikuwa bora, hatukutumia ubora huo kupata matokeo na kuna nyakati mpinzani wetu alikuwa bora, akatumia ubora wake kupata matokeo.”
Ahmed Ally ataja eneo linalohitaji maboresho
Ahmed Ally pia ameeleza kuwa Simba bado inahitaji kufanya maboresho katika baadhi ya maeneo ya kikosi, akilitaja zaidi eneo la ushambuliaji.
“Nikiri tu kuwa timu yetu inahitaji maboresho, hasa kwenye eneo la ushambuliaji. Hilo ndilo eneo pekee mpaka sasa bado hatujafanya vizuri.”
Licha ya kipigo hicho, amewataka mashabiki wa Simba kutokata tamaa, akisisitiza kuwa msimu bado ni mrefu na timu ina michezo 30 ya Ligi Kuu Tanzania Bara mbele yake.
“Tusikatishwe tamaa wala tusijipoteze njiani. Tunayo safari muhimu sana mbele yetu, mechi 30 za Ligi Kuu.”
Ahmed Ally amehitimisha ujumbe wake kwa kuwataka Wana Simba kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar.
“Poleni Wana Simba wenzangu. Nguvu sasa tuielekeze kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Kagera Sugar.”
Kwa Simba, mchezo huo wa Ligi Kuu utakuwa nafasi ya kuanza ukurasa mpya baada ya kupoteza dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni