Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yusuph Masauni, ameitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupewa mamlaka na uwezo zaidi wa kisheria na kiutendaji ili kuimarisha usimamizi wa mazingira nchini.
Masauni ameyasema hayo wakati akiongoza zoezi la usafi katika Soko la Buguruni jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mazingira ya jiji yanakuwa safi na salama kwa wananchi.
Amesema Dar es Salaam ni kitovu cha shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini, hivyo kuna umuhimu wa kulinda mazingira dhidi ya changamoto za uchafuzi wa hewa, kelele, ukataji miti na upungufu wa maeneo ya kijani.
Waziri Masauni pia amesisitiza kuwa maelekezo ya Rais kuhusu kuitenga Jumamosi kuwa siku ya usafi bado yapo na yanapaswa kuendelea kutekelezwa kwa kudumu ili kujenga utamaduni wa usafi na utunzaji wa mazingira katika jamii.
Aidha, ameitaka NEMC kuhakikisha inasimamia ipasavyo sheria na taratibu za mazingira, ikiwemo kuchukua hatua dhidi ya watu na taasisi zinazokiuka masharti ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Masauni amesema viwanda vinapaswa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira na kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti uchafuzi wa hewa na maji. Pia amesisitiza umuhimu wa kudhibiti kelele, mitetemo pamoja na matumizi yasiyofaa ya mifuko ya plastiki.
Amesema usimamizi bora wa mazingira ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zinazohusika, sekta binafsi na wananchi ili kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni