Breaking


Alhamisi, 15 Oktoba 2026

NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAPUNGUZA GHARAMA, KUOKOA MUDA NA KULINDA AFYA NA MAZINGIRA


Wakala wa Nishati Vijijini-REA umeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutoa ruzuku inayowawezesha wananchi wa Mkoa wa Tanga kupata mitungi ya gesi ikiwa na gesi na vifaa vyake kwa shilingi 17,500 pekee, hatua iliyopokelewa kwa furaha na wanawake walioahidi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Akizungumza katika maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Mhandisi David Malima kutoka REA, amesema mpango huo unalenga kupunguza gharama za awali za ununuzi wa vifaa vya gesi na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kutumia nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa kupitia ruzuku hiyo, wananchi wanapata mitungi ya gesi ikiwa imekamilika pamoja na vifaa vyake kwa bei nafuu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Akizungumza baada ya kunufaika na ruzuku hiyo, mkazi wa Tanga, Aziza Ramadhani, ameipongeza REA kwa kuwapa wanawake fursa ya kupata mitungi ya gesi kwa gharama nafuu, akisema hatua hiyo itawasaidia kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Aziza, amewahimiza wanawake wengine kuchangamkia fursa hiyo, huku akiishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira yanayowezesha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.

Hakuna maoni: